Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Nakuru Mary Mbugua amesema kuwa nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na waziri wa ugatuzi aliyejiuzulu Anne Wairugu ilifaa kupewa mwanamke.

Mbugua amesema kuwa Rais Uhuru Kenyatta aliwakosea wanawake wa Kenya kwa kumteua waziri mwanamume kuchukua nafasi iliyowachwa wazi na Waiguru.

Akiongea Alhamisi mjini Molo Mbugua alisema kuwa wanawake wamedhihirisha jinsi wanavyoweza kufanya kazi bora na ni makosa kwa Rais kupunguza idadi ya wanawake katika baraza la mawaziri.

“Sisi kama wanawake tulitarajia kuwa rais Kenyatta angemteua mwanamke kuchukua nafasi ya Waiguru kwa heshima ya wanawake wa Kenya. Kumteua mwanamume kuchukua nafasi hiyo inadhihirisha kuwa Rais Kenyatta hawajali wanawake,” alisema Mbugua.

Mbugua aliwataka wabunge wanawake katika mabuneg yote mawili kuitisha kikao na rais Kenyatta ili kuwasilisha tetesi zao kwake.

“Wawakilishi wa wanawake katika bunge la taifa na Seneti wanafaa kufikiria kuhusu kuitisha kikao na Rais Kenyatta ili tumweleze masikitiko yetu na tumwambie kuwa amekiuka katiba kwa kupunguza idadi ya mawaziri wanawake katika baraza lake,” akasema.

Aidha alisema kuwa nafasi iliyoachwa na Charity Ngilu katika wizara ya ardhi pia ingejazwa na mwanamke.

“Hata nafasi ya Ngilu ingepewa mwanamke lakini rais akaamua kumpa mwanamume na hapo kama wanawake tunahisi kwamba tumeibiwa,” akasema,.