Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu Catherine Nyamato ameyashtumu mashirika yasiyokuwa ya serikali kwa kutumia mbinu zisizo na makali kudhibiti ukeketaji.
Akihutubu katika eneo la Bogichora siku ya Jumatano, Nyamato alisema kuwa kampeni za mashirika hayo huandaliwa katika sehemu za mijini hali inayotenga sehemu za mashambani, ilhali sehemu hizo ndizo huripoti visa vingi vya ukeketaji.
"Mimi ni mwanaharakati wa masuala ya kushinikiza kutokeketwa kwa wasichana, na nafikiri kuwa kampeni zinazofanywa na mashirika ya jamii mijini haziwezi saidia kupunguza visa vya ukeketaji kwa kuwa visa vingi vya ukeketaji huripotiwa vijijini na wala sio mijini," alisema Nyamato.
Nyamato aliongeza kwa kuhimiza mashirika hayo yakutetea haki za binadamu kuiga mfano wa mashirika ya kaunti ya Kisii yanayowapa mafunzo wasichana juu ya kuvuka daraja la utu uzima pasina kukeketwa.
"Ni vizuri mashirika haya yajue kuwa mambo yamebadilika siku hizi na hamna mwafaka wowote utakao afikiwa kwa kufanya maandamano barabarani dhidi ya ukeketaji. Sharti mashirika hayo yawape wasichana mafunzo kuhusiana na vile watakavyo vuka daraja la utu uzima pasina kuketwa kama vile mashirika ya Kisii yanavyofanya,” alisema Nyamato.
Hata hivyo, Nyamato alidhihirisha imani kuwa ukeketaji wa wasichana utaangamizwa miongoni mwa jamii ya Abagusii kwa kuwa wakazi wamepata ufahamu kuhusiana na madhara ya ukeketaji.