Share news tips with us here at Hivisasa

Baada ya mwenyekiti wa kamati ya ardhi nchini Mohammed Swazuri kuwataka wakazi wa eneo la Changamwe kuhama kutoka mashamba ya wenyewe, Maskwota katika eneo la hilo wameitaka serikali kuwapa shamba kama maskwota wengine katika maeneo mengine.

Wakazi hao wakiongea na mwandishi huyu siku ya Jumanne katika eneo la Changamwe walisema kuwa serikali ya kitaifa sharti iwafanikishie haki yao ya kuwapa mashamba kama wakenya wengine.

Akiongea kwa niaba ya maskwota hao, Robnison Mwame alisema kuwa kwa mda mrefu wamekuwa wakikaa kwenye eneo hilo na kuambiwa watoke ni kama kuwanyima kuishi.

Aidha, aliongeza kuwa wao wana watoto na familia ambayo inawategemea, hivyo basi serikali ya kaunti na ile ya kitaifa sharti ifanye hima na kuliangazia swala hilo kwa haraka.

“Sisi hapa tunadhulumiwa wazi na si haki kamwe kuendelea kupewa vitisho kila mara tukiwa hapa na serikali zote mbili sharti zifanye hisani na kulingazia suala hili kwa haraka," alisema skwota huyo.

"Tuna watoto wengine hapa, wamekulia hapa, hivyo serikali kupitia kwa wizara husika sharti ionekane kutekeleza kwa vitendo sababu kuna maskwota wengine walipewa ardhi, mbona sisi tusipewe,” aliongezea.

Hata hivyo, bado hakuna dalili kuwa jamii hiyo itapata kupewa fidia wala kutafutiwa ardhi mbadala ikizingatiwa kuwa tayari mwenyekiti wa tume ya ardhi nchi Mohamed Swazuri aliwataka wahusika kuondoka eneo hilo.