Mkurugenzi wa hoteli za Heritage, ambaye pia ni mwenyekiti wa muungano wa utalii Pwani Mohamed Hersi ameyataka mataifa ya Uingereza, Marekani na Ufaransa kuondoa marufuku kwa raia wake kuzuru kisiwa cha Lamu akisema kuwa kisiwa hicho hakijakumbwa na tishio la kiusalama licha ya kuekwa marafuku hayo.
Hersi alisema kuwa kwa sasa hali ni shwari kwa watalii kuzuru kwani serikali imeimarisha hali ya usalama katika kisiwa hicho na sehemu za karibu.
Marufuku sawia na hiyo iliondolewa mjini Mombasa, Diani, Malindi na Watamu, huku watalii wengi wakitarajiwa msimu huu wa krismasi.
Katika barua kwa vyombo vya habari siku ya Ijumaa wakati kisiwa hicho kiliadhimisha sherehe za kitamaduni za kila mwaka, Hersi alisema kuwa wako katika hali salama na hoteli zao ziko tayari kuwapokea watalii kwa wingi.
Afisa huyo aliongezea kuwa kisiwa hicho kinategemea sana utalii, na marufuku hiyo iliyowekwa mapema mwaka huu baada ya kushuhudiwa mashambulio ya kigaidi Mpeketoni imeathiri pakubwa uchumi sio tu wa kisiwa hicho bali Kenya kwa jumla.