Waziri wa elimu Fred Matiang’i ameahidi kuwa atahakikisha uwanja wa shule ya msingi ya Naka haujanyakuliwa. Matiang’i alikuwa akiongea kwenye shule hiyo siku ya Jumatatu baada ya kufanya ziara ya ghafla.
Waziri huyo alisikitika baada ya kupata habari kuwa kuna mzozo wa ardhi hiyo kati ya shule hiyo na bwenyenye mmoja.
“Mimi nitahakikisha shule mnapata uwanja wenu ili mwendeleze ujenzi wenu. Nitashirikiana na maafisa kutoka Nairobi kuhakikisha shule imepata haki,” Matiang’i alisema.
Shule ya Naka imekuwa na mvutano na mwekezaji mmoja wa kibinafsi mjini Nakuru ambaye anadai umiliki wa uwanja huo. Mapema mwaka jana wanafunzi na wazazi wa shule hiyo walilazimika kufanya maandamano kupinga unyakuzi wa ardhi hiyo.