Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewataka mawaziri wake kufanya miradi ya maendeleo kulingana na pesa zilizotengewa miradi hiyo.
Kulingana na Nyagarama, miradi mingi haikamiliki kwa muda unaofaa, baada ya miradi hiyo kufanywa bila kufuata pesa zilizotengewa miradi husika, jambo ambalo limesababisha miradi mingi kutokamilika inavyostahili.
Akizungumza siku ya Jumatano katika majengo ya kaunti ya Nyamira wakati mawaziri wake walikuwa wanawasilisha ripoti kwa gavana Nyagarama jinsi miradi ya maendeleo inaenda kufanywa katika sehemu mbalimbali za kaunti, gavana aliwataka mawaziri kutumia pesa vizuri.
“Baadhi ya wakazi na wanasiasa husema serikali yangu hutumia pesa za maendeleo vibaya, madai ambayo si ya ukweli. Naomba maafisa wangu wote kufanya miradi ya maendeleo kulingana na pesa zile zimetengewa miradi hiyo ili kukamilika kwa muda unaofaa,” alisema Nyagarama.
Nyagarama katika siku za hivi karibuni ameonekana kupigania maendeleo huku akitoa onyo kwa maafisa ambao hawafanyi kazi inavyostahili.
Aidha, gavana huyo aliahidi kuhakikisha kufanya miradi mingi ya maendeleo katika kaunti yake ili wakazi kunufaika kutokana na maendeleo hayo.
“Naomba tufanye kazi pamoja ambayo ni ya maendeleo katika sehemu zote za kaunti yetu ya Nyamira,” aliongeza Nyagarama.