Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Nyamira Alice Chae ameahidi kuwafadhili kimasomo wanafunzi 10 mayatima katika shule ya msingi ya Risa iliyoko wadi ya Gesima, Kaunti ya Nyamira.
Wanafunzi hao 10 mwaka ujao watakuwa darasa la nane baada ya kufanya mitihani yao vizuri katika darasa la saba mwaka huu kulingana na ripoti ambazo mwakilishi huyo alikabidhiwa kutoka shule hiyo.
Kulingana na mwakilishi huyo, amejitolea kuwaendeleza hadi wamalize kidato cha nne ikiwa watapita katika mitihani ya darasa la nane mwaka ujao ili nao waje kujisaidia nyakati zijazo.
Alikuwa akiongea siku ya Jumatatu katika wadi hiyo ya Gesima, huku akisema mayatima wanastahili kusaidiwa kwa njia zote kwani hawana wa kuwasaidia
Ata hivyo, aliomba wahisani wengine kujitolea kutoa msaada wao kwa mayatima ambao wako na mahitaji ya masomo lakini hawana wa kuwaendeleza.
Wakati huo huo, Chae alipongeza mahakama kwa kuwashtaki wanawake watano katika kaunti hiyo ya Nyamira kwa kukiuka sheria kwa kuwapeleka wanao wasichana katika tohara, jambo ambalo haliruhisiwi na sheria.
“Tunaomba haki itendeke kwa watoto wasichana katika eneo la Kisii, na ninaomba wanawake wale waliofikishwa mahakamani washtakiwe ili iwe funzo kwa wengine,” alisema Chae.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kupambana na tohara kwa wasicha Linah Kilimo, asilimia 98 ya wanawake huwapeleka wanao wasichana katika tohara katika eneo la Kisii.