Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko pamoja na wanawake wengine wamekashifu maneno aliyoongea seneta wa Nairobi Mike Sonko dhidi ya Gavana wa Mombasa siku ya Jumamosi kwenye mkutano uliohudhuriwa na rais Uhuru Kenyatta.
Mishi amemtaka Sonko kuheshimu upinzani, hususan viongozi wa upinzani katika ukanda wa Pwani, na kumpa changamoto Sonko kuenda kupigania uongozi wa Pwani iwapo ataweza lakini sio kukashifu viongozi wa eneo hilo.
Aidha maandamano mbali mbali yalifanyika siku ya Jumapili jijini Mombasa, huku wale wanaoegemea upande wa JAP wakimuunga Sonko na kubeba mabango ya kumtaka kuwania ugavana wa Mombasa.
Nao wafuasi wa ODM walibeba mabango ya kumtaka Sonko awachane na Joho, huku mabango hayo yakiwa yameandikwa 'Joho ndiye gavana wetu'.
Haya yanajiri baada ya Sonko kumkejeli na kumkemea Gavana Joho kwenye mkutano uliohudhuriwa na Rais Kenyatta katika eneo la Shika Adabu, eneo bunge la Likoni, siku ya Jumamosi.