Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko amewahimiza maafisa wa polisi wanaowakabili walanguzi wa dawa za kulevya kuimarisha mbinu zao ili kuwanasa washukiwa.

Mboko alisema kuwa itakuwa vigumu kwa maafisa hao kufanikiwa ikiwa watasalia na mbinu za kawaida kwani washukiwa tayari wameibua mbinu mpya za kusafirisha dawa hizo, ikiwemo kutumia baiskeli ili kukwepa mtego wa maaafisa wa usalama.

“Walanguzi wa mihadarati wamegundua mbinu wanazotumia walinda usalama kuwakalibi. Kwa hivyo, maafisa wetu lazima nao watumie mbinu mpya ili wafanikiwe,” alisema Mboko.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, kiongozi huyo alitaja Likoni, Kisauni, Changamwe na Jomvu kama maeneo yaliyoathirika zaidi na dawa za kulevya.

Alisema kuwa idadi kubwa ya walioathirika katika eneo hilo ni vijana wenye umri mdogo.

Mboko alisema kuwa licha ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza vita vikali dhidi ya walanguzi wa dawa za kulevya na kuonya kuwa wahusika watachukuliwa hatua kali za kisheria, bado biashara hiyo haramu ingali inatekelezwa nchini, hususan eneo la Pwani.