Wanawake wa Kaunti ya Mombasa wamehimizwa kujiunga katika makundi ili kufaidika na hazina ya akina mama iliyozinduliwa na serikali ya kaunti hiyo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumapili, Mwakilishi wa wanawake katika kaunti hiyo Bi Mishi Mboko alisema kuwa changamoto za kiuchumi zinazowakumba akina mama katika kaunti hiyo zitakabiliwa.
Mboko aidha aliongeza kuwa hazina hiyo itaimarisha wanawake na jamii ya kaunti hiyo kwa kiwango kikubwa maishani, kwani itawafungulia nafasi nyingi za kibiashara.
Kiongozi huyo amewataka akina mama kushirikiana katika shughuli za kibiashara ili kubadili hali ya maisha, huku akimtaka Gavana wa Kaunti hiyo Hassan Ali Joho kuhakisha kuwa zabuni zinazotolewa na kaunti hiyo, asilimia 30 zinawaendea wanawake, vijana na walemavu.
“Tafadhilini akina mama, wakati ni sasa wa kujiunga na makundi ya kimaendeleo ili kufaidika na hazina ya wanawake iliyozinduliwa na serikali ya Kaunti ya Mombasa, na kubadili hali yao ya maisha,” alisema Mboko.