Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Mombasa, Mishi Mboko, anadai kuwa hatua ya serikali ya Jubilee kumteua waziri wa utalii Najib Balala, na waziri wa madini Dan Kazungu katika baraza la mawaziri ni ya kuwafumba macho wakazi wa Pwani.

Mboko anahoji kuwa ni jambo la kushangaza kuona eneo la Pwani likiwakilishwa na waziri wawili pekee katika serikali licha ya eneo hilo kuwa miongoni mwa mikoa mikubwa nchini.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano kwenye hafla ya kuizindua rasmi barabara ya Fidel Odinga, iliyoongozwa na kiongozi wa mpinzani Raila Odinga, Mboko alisema kuwa Pwani haifai kutengwa licha ya kutompigia kura kwa wingi Rais Kenyatta katika uchaguzi uliopita.

"Kila mtu anajua kua Pwani ilimpigia kura Raila Odinga lakini hiyo haimanishi kua sasa tunafaa kutengwa, kupiga kura ni haki na ni demokrasia ya mtu binafsi hivyo hafai kuhukumiwa kutokana na uhamizi wake," alisema Mboko.

Aidha, ameuwambia mrengo wa Jubilee kuwa wanasiasa wa Pwani wanamsimamo thabiti na kuwa hawawezi shawishiwa kwa urahisi kuvihama vyama vyao.

Mboko vilevile alisema kuwa Pwani itasalia kuwa ngome ya mrengo wa Cord na kuwa wanasiasa wanaolenga kuugura mrengo huo wawe tayari kwa mawimbi ya kisiasa katika uchaguzi wa 2017.