Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko amesema kuwa atajitolea kuona kuwa wanawake katika kaunti hiyo wanashirikishwa kikamilifu katika maendeleo.
Akiongea katika eneo la Treasury, jijini Mombasa kwenye hafla ya kuyachangia makundi ya wanawake siku ya Jumapili, Mboko aliwapa changamoto wanawake kuamka na kuanza kujihusisha na shughuli ambazo zitawapa mapato badala ya kukaa na kusubiria tijara kutokana na shughuli za wanaume zao na kusema kuwa wakati wa wanawake kujitegea umefika.
Mwakilishi huyo alisema kuwa atapigania haki zote zinazowalenga kina mama katika kaunti hiyo kama vile kupata zabuni za kutoka kwenye kaunti kama inavyoweka wazi katiba mpya.
Alielezea umuhimu wa kina mama wa kuunda makundi ya kujiendeleza kiuchumi na kuongeza kuwa makundi haya yatasaidia kupata kandarasi kwa urahisi na pia kupewa zabuni badala ya kuwa mbalimbali.
“Makundi ya kina mama yanawapa nafasi ya rahisi ya kutangamana na kujadili masuala ya masuala ya kiuchumi, kwa hivyo nawahisi mje pamoja,” aliwapa changamoto mwakilishi huyo.
Kwenye hafla hiyo kulihudhuriwa viongozi mbalimbali wa kutoka kaunti ya Mombasa wakiongoza na gavana wa kaunti hiyo Ali Hassan Joho ambaye alionyesha kujitolea kuona kuwa wanawake pamoja na wakaazi wanapata maendeleo na kushiriki kwenye mchakato wa kuinua viwango tofauti na kuchangia kuimarika kwa uchumi wa kaunti hiyo.