Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko amesema kuwa ulanguzi wa dawa za kulevya unaendelea kukita mizizi mjini Mombasa licha ya rais Uhuru Kenyatta kuamrisha vyombo vya usalama kukabiliana na hali hiyo.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Mboko alisema kuwa walanguzi wa dawa za kulevya wamebadili mbinu ya kusafirisha dawa hizo, na hutumia baskeli kama njia mojawapo ya kukwepa maafisa wa usalama.

Amesema kwamba kwa sasa biashara hiyo imeenea zaidi katika maeneo ya Likoni, Kisauni, Changamwe na Jomvu, na lazima maafisa wa usalama kuwakabili na kuwanasuru vijana wadogo waliojitosa katika jinamizi hilo.

Mboko amedokeza kuwa watumizi na waraibu wa mihadarati idadi kubwa imetorokea kusini mwa Pwani, hasa maeneo ya Ukunda, Kwale, Diani na Msambweni kuendeleza biashara hiyo haramu.

“Tunaitaka idara ya usalama kurejelea tena oparesheni ya kuwasaka vijana waliojitosa katika janga la mihadarati na kupelekwa katika vituo vya matibabu, na walanguzi wote pia watiwe nguvuni ili vijana wetu wabadiliki kifikra,” alisema Mboko.

Aidha, Mboko amesema maskani za watumizi wa mihadarati zimerejea kama kawaida hata baada ya maafisa wa usalama kuwakabili watumizi na kupelekwa katika vituo vya matibabu.

Ametaja maeneo ya Magodoroni, Bamburi, Mwandoni Blue Bench, Bombolulu, Mtwapa (Mti ni Pesa), Shanzu, Likoni (Shelly Beach) na Changamwe (Magongo) kama wameneo yanayotumika kuuza dawa za kulevya.