Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Mombasa Bi Mishi Mboko amewakashfu viongozi wa kisiasa waliyotangaza kuhama chama cha ODM na kujiunga na Jubilee.

Kulingana na Mboko viongozi hao wameonyesha wazi kuwa sio wanachama halisi bali walijiunga na ODM kwa misingi yao binafsi na kuhama chama hicho ili kujiunga na Jubilee ni kutokana na tamaa zao ya kutafuta kupata ufadhili katika uchaguzi.

Akiwahutubia wakaazi wa eneo la Likoni katika shule ya msingi ya Mrima wakati wa ufunguzi wa mradi wa maji safi na vyoo vya kisasa siku ya Alhamisi, Mboko alisema kuwa kutangaza kwa viongozi hao kukihama chama hicho kamwe hawatatatiza mipangilio ya chama hicho.

“Sisi kama wanachama halisi wa chama cha ODM kamwe hatujatatizwa na baadhi ya viongozi wasaliti walitangaza kuhama chama cha ODM na tutaendelea kusalia wanachama ngangari hadi tuchukue uongozi wa taifa hili,” alisema Mboko.

Mboko aliwataka wakaazi wa eneo hilo kuunga mkono juhudi za chama cha ODM na mrengo mzima wa Cord ili kuhakikisha kuwa serikali ya Jubilee inaondolewa madarakani wakati wa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2017.

“Tunawaomba wakaazi wa Likoni kusimama kidete pamoja na sisi viongozi wenu wa ODM ili kuhakikisha kupiga kura kwa wingi na kubadilisha uongozi wa nchi hii,” alisema Mboko.