Gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua amewahimiza wananchi wa kaunti hiyo ambao tayari wana vitambulisho vya kitaifa kujitokeza na kujisali kupiga kura ili kuwapa fursa ya kuchagua viongozi bora.
Mbugua akizungumza katika wadi ya Nyota, kaunti ndogo ya Kuresoi Kusini siku ya Jumatano wakati wa kuzindua rasmi shughuli hiyo ya usajili wa kura katika kaunti hiyo pia ameelezea kuwa hatua hiyo itawapa wananchi fursa muhimu ya kuchangia katika maendeleo ya maeneo yao kwa kuzingatia viongozi wema.
"Kupiga kura ni muhimu kwa kila mwananchi kwa sababu inawapa fursa sawa ya kuchagua wale viongozi ambao wataleta maendeleo nchini bila ubaguzi au ufisadi. Ni wakati ambao tunahitaji kuwapinga viongozi wenye uchochezi na siasa zisizosaidia eneo hili, na hili litawezekana iawapo kila mmoja atajisajili kuchukua kura," Mbugua alisema.
Gavana huyo pia aliwarai viongozi katika kaunti hiyo kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kupiga kura ili watu wajitokeze kwa wingi.
Zaidi ya watu 700,000 wamesajiliwa kupiga kura katika kaunti ya Nakuru huku Gavana huyo akilenga watu zaidi kujitokeza katika shughuli hiyo.