Share news tips with us here at Hivisasa

Wiki moja baada ya mashirika ya kijamii kuandamana kupinga uongozi wa gavana wa Nakuru Kinuthia Mbugua, shirika moja la kijamii limejitokeza kutetea uongozi wake.

Shirika la Molo Peoples Forum hapo jana lilisema kuwa gavana Mbugua ametekeleza majukumu yake ipasavyo na kuyashtumu yale mashirika yalioandamana kumpinga.

Wakizungumza mjini Nakuru Ijumaa asubuhi viongozi wa shirika hilo walisema kuwa ni unafiki kwa watu kuona makosa madogo yanayotokea badal ya kuona makubwa yaliyofanywa na Gavana Mbugua.

Mwenyekiti wa shirika hilo Rose Wanja, alisema kuwa makosa yanayolimbikiziwa gavana Mbugua yalitekelezwa na maafisa wake bali si yeye mwenyewe.

“Ukiona yale mambo anasemekana kufanya si yeye aliyeyafanya bali ni maafisa wake katika serikali na hili haliwezi kufanya watu kumtaka gavana kuondoka,Kama waziri amekosa huwezi kumuambia rais aondoke bali Yule waziri bdiye atakaye ondoka,” alisema Wanja.

Aliwataka wakaazi wa Nakuru kuangazia maendeleo aliyoleta Mbugua kufikia sasa na kukoma kuchochewa na wanasiasa wanaopinga utawala wake.

“Kuna watu ambao hata mazurri yafanyike hawawezi kuona ila kazi yao ni kuwachochea tu watu na kufadhili maandamano dhidi ya gavana lakini tunawataka wananchi wa Nakuru kuwa macho na kujihadhari an watu kama hao ambao kazi yao ni kucheza siasa chafu,” akasema.

Mratibu wa mipango katika shirika hilo Godfrey Koech alisema kuwa wataandaa maandamano ya kumuunga gavana Mbugua mkono na kuwtaka wananchi wapenda maendeleo kushirikiana nao.

“Waliandamana kupinga gavana na sisi pia tutaandamana kumuunga mkono na kusifiakazi yake na tunawataka watu wa Nakuru kujiunga nasi kufanya hilo hivi karibuni,” alisema Koech.