Share news tips with us here at Hivisasa

Wanafunzi katika shule za msingi za umma katika eneo bunge la Nakuru Magharibi sasa wana sababu ya kutabasamu kwani hivi karibuni tatizo la ukosefu wa maji kwenye shule hizo litatatuliwa.

Akizungumza kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Jumatatu mjini Nakuru, Mbunge wa eneo bunge hilo, Samwel Arama, alisema kuwa atahakikisha visima vinachimbwa katika shule zote za umma za msingi katika mwaka ujao wa kifedha wa 2016/2017 ili kukabiliana na tatizo hilo la ukosefu wa maji.

Arama alisema kuwa ingawa baadhi ya shule katika eneo bunge hilo zinapata maji yanayosambazwa na kampuni ya Nawasco, huduma hiyo husitishwa kwa wakati mwingine baada ya wazazi kutatizika kugharamia malipo yake.

“Nataka mabwawa ya maji yachimbwe katika shule zote za msingi za umma zilizo katika eneo bunge langu. Hilo ni pendekezo langu katika mwaka ujao wa kifedha wa 2016/2017. Hii ni kutokana na kuwa shule nyingi zilizo katika eneo bunge la Nakuru Magharibi zinakabiliwa na uhaba wa maji,” alisema Arama.

Aliongeza, “Kwa wakati mwingine, shule hizo hupata maji yanayosambazwa na kampuni ya maji wa Nawasco lakini wazazi hushindwa kumudu gharama yake.”

Kulingana naye, mradi huo utaanzishwa katika Shule ya Msingi ya Nakuru West na kisha kuelekezwa katika shule zingine za msingi za umma zilizo kwenye eneo bunge hilo, huku akidhibitisha kuwa wakaguzi wa eneo ambalo kisima hicho kitachimbwa watafika shuleni humo hivi karibuni.