Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kisii Mary Otara ameombwa kuwaleta pamoja viongozi wa eneo hilo ili kutafuta mbinu ya kuwaondoa watoto wakike ambao wanafanya ukahaba mjini Kisii.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa idadi kubwa ya wasichana ambao wanafanya ukahaba mjini humo wako chini ya umri wa miaka 20, jambo ambalo si la kufurahisha kwani wengi wao hawakumaliza hata darasa la nane kulingana na uchunguzi.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika eneo la Marani, bunge la Kitutu Chache Kaskazini, mkurugenzi wa chuo kikuu cha African Nazarene Norah Nyamwamu alisema sharti mbinu zitafutwe kuwaokoa wasichana hao.
Nyamwamu alimuomba Mwakilishi wa wanawake Otara kuwaleta viongozi pamoja kutatua hali hiyo ya ufuska unaozidi kukithiri.
“Wasichana ambao hufanya ukahaba mjini Kisii ni watoto ambao hawakumaliza shule na wamejihusisha katika vitendo ambavyo si vya kupendeza,” alisema Nyamwamu.
“Ni aibu kama viongozi kuona jambo hilo likiendelea, naomba Mwakilishi wa wanawake Mary Otara awalete pamoja viongozi kutafuta suluhu ya janga hili hapa Kisii,” aliongeza Nyamwamu.
Wakati huo huo, wazazi waliombwa kuwasomesha watoto wakike ili waje kujisaidia siku za usoni kwani masomo ndio msingi katika maisha ya kila mtu katika jamii.