Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi ameishtumu serikali kwa kukosa kuwasaidia vijana wa Pwani kupata ajira licha ya kwamba eneo hilo liko na raslimali nyingi.

Mbunge huyo alisema kwamba licha ya kuwa makao ya Kenya Navy yako Mombasa, bado vijana wa eneo hilo hawapati fursa ya kufaidi nafasi za kazi.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatano, Mwinyi alidai kuwa wengi wanaopata nafasi za kazi katika sekta hiyo ni watu wanaotoka maeneo mengine, huku vijana wa Pwani wakinyimwa nafasi hizo.

“Jubilee ilisema itawapa vijana kazi. Hapa tukona Kenya Navy lakini watoto wetu wanaangaika bila kupewa nafasi,” alisema mbunge huyo.

Kiongozi huyo alidai kuwa tangu serikali ya Jubilee kuingia mamlakani, vijana wa Pwani wamekuwa wakinyimwa kazi katika Bandari ya Mombasa, ambayo ilitarajiwa kuwafaidi zaidi watu wa eneo hilo.

Matamshi yaliungwa mkono na kiongozi wa Cord Raila Odinga, aliyetaja serikali ya Jubilee kama yenye ahadi za uongo kwa wananchi.

Raila aliongeza kwamba vijana wa Pwani wanafaa kusimama imara na kuunga mkono muungano wa Cord, huku akisema wako tayari kuikomboa Pwani kutoka katika umaskini unaoendelea kuzorotesha maendeleo.

“Vijana mliambiwa mtapewa kazi, huku wanawake mkiambiwa mtapewa mikopo, lakini ahadi hiyo bado haijatimizwa. Siasa ni kama vita wala siasa sio harusi, kwa hivyo vijana tusimame na tupambane ili tujikomboe,” alisema Odinga.