Kuna njama ya kuwatia nguvuni gavana wa Kilifi Amason Kingi na mwakilishi wa wanawake Aisha Jumwa kutokana na kuhusika kwao kwenye kampeni za eneo bunge la Malindi, kulingana na mbunge wa Ndhiwa Agostino Neto.
Akizungumza mjini Naivasha kaunti ya Nakuru mnamo Ijumaa, mbunge wa Ndhiwa Agostino Neto aidha alisema wakenya hawana imani tena na tume huru ya uchaguzi nchini IEBC.
Neto alisema kuwa wakenya hawana imani na IEBC kwamba itasimamia uchaguzi huru na wa haki mwaka wa 2017, matokeo yake yakiwa ni idadi ndogo ya wakenya wanaojitokeza kujiandikisha kama wapiga kura.
Mbunge huyo alisema kuwa hatua ya kumnyima gavana wa Mombasa Hassan Joho walinzi ni njia moja ya kulipiza kisasi kutokana na uchaguzi wa Malindi.
“Watu wanapoteza azma ya kwenda kujiadikisha kwa sababu wanahisi hata wakichaguana huenda kutakuwa na wizi wa kura,”Neto alisema.
Alisema hatua ya mratibu wa kanda ya Pwani Nelson Marwa kuwaondoa askari hao ilikuwa mfano wa kurudisha Kenya kwenye enzi za zamani licha ya kuwepo kwa katiba mpya.
“Tunajua kwamba kumekuwa na matatizo ya mashamba na makundi haramu kama MRC Mombasa, lakini wakati tunafanya mambo kama viongozi tukumbuke kwamba uchaguzi mkuu unakaribia na chochote chaweza kugeuzwa kuwa makabiliano,” mbunge huyo alisema.