Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Masaba Timothy Bosire amejitokeza kumshtumu vikali naibu rais dhidi ya kuingililia masuala ya kisiasa ya eneo la Gusii. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubu katika shule ya upili ya wavulana ya Nyambaria siku ya Jumapili wakati wa kuzindua rasmi kinyang'anyiro cha mchezo wa soka, Bosire alisema kuwa eneo la Gusii ni ngome ya ya muungano wa Cord, huku akimshtumu Ruto kwa kuendelea kuwalazimisha baadhi ya viongozi wa kisiasa kujiunga na mlengo wa Jubilee. 

"Naibu Rais William Ruto amekuwa akiifunza jamii ya Abagusii kuhusiana na maamuzi ya kisiasa wanayostahili kuyatekeleza ilhali ameshindwa kuthibiti malumbano ya kisiasa katika eneo lake la Bonde la Ufa, na wacha afahamu kuwa tumechoshwa na siasa za kuwagawanya wakenya," alisema Bosire.

"Kwa kweli iwapo kuna miradi ya maendeleo serikali yafaa kututekelezea sharti ifanye hivyo kwa kuwa sisi sote ni wakenya hata kama twaunga mkono milengo tofauti ya kisiasa," aliongeza Bosire. 

Bosire aidha alimshtumu Ruto kwa kutumia mamlaka yake ili kuhujumu maendeleo katika eneo la Gusii, huku akiwahimiza watu wa jamii ya Abagusii kuunga mkono mlengo wa upinzani Cord. 

"Ni jambo la kushangaza kwamba Ruto anatumia mamlaka yake ili kuhujumu miradi ya maendeleo katika maeneo mengi nchini na yafaa ajue kuwa sio lazima kila mwananchi aiunge mkono serikali kwa kuwa hili ni taifa huru na ndio maana nawahimiza watu wa jamii ya Abagusii kuunga mkono mlengo wa Cord," aliongezea Bosire.