Mbunge wa Lamu Magharibi Julius Ndegwa na wanachama 6 wa hazina ya ustawishaji maeneo bunge wameitaka mahakama kutupilia mbali kesi ya ufisadi inayomkabili kwa kile wanachodai kuwa mahakama ya Mombasa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa mujibu wa katiba.
Kupitia wakili wao Gerad Magolo, siku ya Jumatano, waliambia mahakama kuwa kesi hiyo haipaswi kusikilizwa katika mahakama ya Mombasa ikizingatiwa tukio hilo lilitokea katika kaunti ya Lamu.
Magolo alisisitiza kuwa kesi hiyo inafaa kusikilizwa katika Mahakama ya Lamu ili kutoa nafasi kwa wakazi wa Lamu kuhudhuria vikao vya kesi hiyo ikizingatiwa wao ndio waathiriwa wakubwa.
Ombi hilo limepingwa vikali na naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Alexendra Muteti kwa kusema kuwa Mahakama ya Mombasa ina uwezo kikatiba kusikiliza kesi hiyo.
Mbunge wa Lamu Magharibi Julius Ndegwa na wanakamati 6 wa hazina ya ustawishaji wa maeneo bunge CDF wanatuhumiwa kutumia vibaya shilingi milioni 1.6 zilizokuwa zimetengewa ujenzi wa kituo cha kutibu mifugo eneo la Witu.