Mbunge wa Makueni mjini Dan Maanzo amejitokeza kuishtumu vikali serikali ya Jubilee kwa kuendelea ‘kupalilia’ ufisadi serikalini.
Akihutubu kwenye hafla ya mazishi ya nduguye Ben Momanyi katika kijiji cha Nyainagu eneo bunge la Borabu, kaunti ya Nyamira siku ya Jumatatu, Maanzo alisema kuwa serikali ya Jubilee ndio serikali fisadi zaidi kuliko serikali za hapo nyuma.
Aidha alihoji kuwa isingekuwa mlengo wa Cord, aliyekuwa waziri wa ugatuzi Anne Waiguru angelikuwa bado akihudumu kama waziri.
“Jubilee ni serikali ambayo imewafeli pakubwa wakenya hasa kwa kuendelea kuruhusu maafisa wafisadi kuhudumu serikalini maana ni wazi kwamba aliyekuwa waziri wa ugatuzi Anne Waiguru angekuwa bado serikalini isingekuwa Cord,” alisem mbuge huyo.
Mbunge huyo wa chama cha Wiper aidha alihoji kuwa serikali ya Jubilee imeshindwa kuwahakikishia wakenya usalama wao, huku akirejelea kisa cha hivi karibuni ambapo idadi isiyojulikana ya wanajeshi waliuwawa kule Alle Adde, nchini somalia.
“Usalama ndio kigezo muhimu serikali yeyote duniani huapa kuwahakikishia wananchi wake inapotwikwa mamlaka ya kuongoza, ila kwa serikali ya Jubilee kwa kweli imefeli pakubwa kwa maana inawezekanaje kwamba wanajeshi wakenya wanaweza uawa na wanamgambo wa Alshabaab bila hata ya serikali kujaribu kulidhibiti kundi hilo," aliongezea Maanzo.