Wakazi wa eneo la Nyakeore katika eneo bunge la Mugirango Magharibi wamepata sababu ya kutabasamu baada ya mbunge wa eneo hilo James Gesami kufungua rasmi shule ya walemavu katika eneo hilo.
Akihutubia wakazi wa eneo hilo kule Nyakeore wakati wa kupokeza rasmi shule hiyo kwa usimamizi wa shule, Gesami alisema kuwa alilazimika kuchukua hatua hiyo ili kuwasaidia wanafunzi walio na ulemavu kupata haki ya masomo sawa na wengine.
Aidha aliwahimiza wazazi walio na watoto walio na ulemavu kutoaibika kuwachukua katika shule za ulemavu ili kupata elimu.
“Nililazimika kuchukua hatua ya kujenga shule hii ili kuwawezesha wanafunzi walio na ulemavu kupata haki yao ya kimasomo kama wale wengine, na ni himizo langu kwa wazazi wenye watoto walio na ulemavu kutowafungia watoto hao nyumbani,” alisema Gesami.
Gesami aidha aliwasihi maafisa wa usalama kuhakikisha kuwa wanaweka mikakati ya kuimarisha usalama vijinini, huku akisisitiza kuwa kituo hicho kitakuwa na hospitali itakayo wahudumia wanafunzi walemavu.
“Tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao, na ni himizo langu kwa maafisa wa usalama kuhakikisha kuwa wanaimarisha usalama vijijini ili kuwahakikishia wananchi usalama wao,” aliongezea Gesami.
Kituo hicho cha walemavu kilijengwa kwa udhamini wa wizara ya elimu na hazina ya maendeleo bunge CDF.