Vurugu ilishuhudiwa siku ya Jumatano kwenye uchaguzi wa chama cha ODM wakati wanachama walijitokeza katika shule ya upili ya wavulana ya Nyamira kuwachagua viongozi mbalimbali wa chama hicho watakaowakilisha kaunti.
Hayo yalijiri baada ya kupatikana kuwa kulikuwa na sajili mbili za majina ya wanachama kutoka maeneo bunge manne, hali iliyopelekea vurugu hiyo na pia kusababisha mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi wa chama cha ODM katika kaunti hiyo Alfred Ndubi kutiwa mbaroni kufuatia makabiliano makali na maafisa wa polisi.
Hata hivyo, uchaguzi huo ulianza saa nane mchana chini ya usimamizi wa mwanachama wa bodi hiyo Dr Evans Kenanda, ambapo mbunge wa eneo bunge la Mugirango Magharibi Dr James Gesami alichaguliwa kama mwenyekiti, mbunge Charles Geni kama katibu, mwakilishi wa wadi ya Manga Peter Maroro kama mweka hazina, Charles Sagwe kama katibu mwandalizi, na Carol Mogere kama mwakilishi wa wanawake.
Mbunge Timothy Bosire, Alice Chae, mwakilishi Zipporah Osoro, Lucy Onsusu, Damaris Mouni miongoni mwa wengine wamechaguliwa kama wajumbe (Delegates) wa chama hicho kwenye kaunti hiyo, na Bosire akawashkuru wanachama wa chama hicho kwa kudhihirisha demokrasia'.