Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir amezindua rasmi mradi wa kupeleka vijana ughaibuni kama njia moja ya kukabiliana na ukosefu wa ajira.
Akizungumza siku ya Ijumaa katika mtaa wa Majengo, Abdulswamad amesema mradi huo unaofadhiliwa na wakfu wa Shariff Nassir utawalipia vijana tikiti za ndege ili kusafiri kupata kazi mbali mbali katika nchi za kiarabu.
Alisema tayari afisi yake imepokea viza 13 kutoka nchi ya Qatar na vijana hao watasafiri kuelekea nchini humo katika muda wa wiki moja, huku akiahidi kusafirisha vijana 300 zaidi katika muda wa miezi mitatu.
Naye Meneja wa benki ya Gulf African tawi la Bondeni Yasser Abdulkarim amewashauri vijana hao kuweka akiba na kuwekeza ili fedha watakazozipata ziwafaidi katika siku za usoni.
Vijana walionufaika na mradi huo wamempongeza Abdulswamad na kutoa wito kwa viongozi wengine kuiga juhudi zake.