Maafisa wa usalama mjini Mombasa wamelaumiwa kwa kile kimetajwa kama kuwahangaisha wenyeji wasio na hatia katika baadhi ya maeneo mjini humo.
Akizungumza mjini Mombasa, mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir, alidai maafisa hao, huwatia mbaroni wenyeji wasio na makosa.
''Huu ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, kila mtu ana uhuru kikatiba kutembea mahali popote wakati wowote bora anaheshimu sheria,'' alisema mbunge huyo.
Mbunge huyo alisema atawasilisha mswada bungeni pindi shughuli za bunge zitakaporejelewa kuhusiana na swala hilo.
Inadaiwa maafisa wa usalama mjini Mombasa, huwakamata watu wanaopatikana katika maeneo yanayosemekana kutumiwa kulangua mihadarati na maeneo ya ukahaba.