Seneta mteule wa kaunti ya Mombasa Emma Mbura sasa anadai kuwa gavana Ali Hassan Joho alimkosea heshima Rais Uhuru Kenyatta kwa kumkosoa mbele ya umma.
Katika mahojiano na gazeti moja la humu nchini siku ya Jumanne, Mbura ameitaja hatua ya gavana Joho ya kumwambia Rais kwamba ''si sawa Bw Rais wewe kuwa Mombasa kwa majuma mawili bila mimi kujua,'' kuwa ya kumdunisha hadhi kiongozi wa nchi.
''Hufai kumnyooshea kidole mkubwa wako mbele ya watu, hiyo ni kumkosea heshima,'' Mbura alisema.
Seneta huyo aidha amemhimiza Joho kumuunga mkono Rais Kenyatta katika jitihada zake za kuufanyia mkoa wa Pwani maendeleo.
Siku ya Jumamosi wikendi iliyopita katika hafla ya kutoa hati miliki kwa wakazi wa shamba la Waitiki, gavana Joho alidai kuwa Rais Kenyatta anamkwepa baada ya Rais kukuwa Mombasa kwa zaidi ya majuma mawili bila kumjulisha.
Hata hivyo, kauli hiyo iliibua hisia kali za kisiasa na kumpelekea Seneta wa kaunti ya Nairobi Mike Sonko kuwataka viongozi wa upinzani kumheshimu Rais, huku akiwataja kama wasaliti wa serikali.