Mwakilishi wa wadi ya Kabatini kaunti ya Nakuru Paul Thuo, amemsuta mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, kwa madai ya kumchafulia jina gavana Kinuthia Mbugua.
Akiongea Jumatano katika shule ya upili ya st. Johns, Thuo alikemea msururu wa mavaamizi ya kisiasa hivi maajuzi kutoka kwa mbunge huyo dhidi ya gavana Kinuthia Mbugua na utendakazi wa serikali yake. Kimani amekuwa akinukuliwa akisema hakuna maendeleo yamefanyika chini ya utawala wa gavana huyo.
“Tunatoa wito kama wawakilishi wa wadi, hatutaki tena kuskia Ngunjiri akipiga siasa chafu za kumchafulia jina gavana na serikali yake. Sisi ndio tuko hapa mashinani, na tumetengeza barabara, tukajenga hospitali, tumejenga soko, pesa za basari zimetoka, na hatupigi kelele kwa sababu hiyo ni kazi ya Kinuthia Mbugua. Yeye kama mjumbe, afanye kazi yake katika bunge la kitaifa,” Thuo alisema.
Aliwataka wakaazi kupuuza alichokiita madai ya Kimani kwamba ‘gavana ni mgeni katika kaunti ya Nakuru’.
“Gavana Mbugua hawezi kuwa na ushawishi mbele ya magavana wengine wote akiwa peke yake. Kesi ipi amewasilisha kortini? Hiyo ni kesi iliyowasilishwa na baraza la magavana nchini chini ya Peter Munya kama mwenyekiti wao. Kimani atunge sheria katika bunge, asaidie sisi kufanya maendeleo, lakini si kuita wanahabari kila kuchao akichafulia viongozi wenzake majina,” Thuo aliongeza.