Share news tips with us here at Hivisasa

Mzozo unaoendelea wa shamba tata la Ng’ati huko Maella umezidi huku wakazi hao Jumanne adhuhuri wakiteketeza nyumba saba zinazomilikiwa na wakurugenzi wa shamba hilo.

Aidha wakazi hao waliojawa na gadhabu wamevamia pia boma za wakurugenzi hao na kuwauwa mifugo wao kabla ya kuharibu tena chakula kilichokuwa kimesalia shambani.

Wakulima hao wanaotaka kuondolewa kwa wakurugenzi hao hii leo wamefunga pia shule zote huku polisi wa kuzima ghasia wakitumwa eneo hilo.

MCA wa eneo hilo Mujina Kariuki aidha ametiwa mbaroni saa chache baada ya ghasia hizo kuzuka huku akidaiwa kuwachochea wakazi hao kufanya vitendo hivyo.

Akizungumza na vyombo vya habari kabla ya kutiwa mbaroni, Mujina amesema kuwa wakazi hao waliamua kuchukua sheria mikononi mwao kwani serikali imekosa kutatua shida iliyoko.

“Wananchi waliamua kuchukua hatua mikononi mwao kwa sababu serikali haisikii kilio chao,” alisema Bw Mujina.

Lakini mwenyekiti wa shamba hilo Patrick Karanja amesema kuwa MCA huyo alikuwa akiingiza siasa katika maswala ya ardhi na alifaa kushtakiwa huku akiongeza kuwa kuna kesi ya uongozi wa shamba hilo mahakamani.