Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya waakilishi wadi katika bunge la kaunti ya Uasin-Gishu wanadai kuwa utawala wa kaunti hiyo unaendeleza ukabila katika kupeana huduma.

Kutokana hali hiyo, viongozi hao wanataka tume ya kitaifa na uiano na utengamano kuingilia kati ili kuchunguza viongozi wanaodaiwa kuendeleza ukabila huo.

Mwakilishi wadi ya Huruma Peter Chomba alisema ukabila huo ni tishio kwa ustawi wa kaunti hiyo haswa katika sekta ya uwekezaji.

Chomba alidai kuwa naibu gavana wa kaunti hiyo Daniel Chemno amekuwa akihangaisha wachuuzi kwa misingi ya kikabila ambapo anataka naibu rais William Ruto kwa ushirikiano na mwenyekiti wa tume ya NCIC Francis Ole Kaparo kuingilia kati ili kunusuru hali hiyo.

“Naibu gavana anayetumia lugha mbaya kwa kuandama wachuuzi na wahudumu wa bodaboda kutoka sehemu za nje ya kaunti hii kwa kuwataka wahame kutoka mjini Eldoret na kurudi katika kaunti za makwao,hali hii inatishia wawekezaji katika sekta ya juakali ambapo ni aibu kwa kiongozi wa kiwango hicho kuendeleza chuki na ukabila,” alisema Chomba.

Chomba alidai kuwa juhudi za gavana wa kaunti hiyo kutafuta wawekezaji zaidi kutoka mataifa ya kigeni hazitazaa matunda iwapo naibu wake ataendelea kuhubiri ukabila.

Madai ya Chomba yaliungwa mkono na kiongozi wa waliowachache katika bunge hilo bw Ramadhan Ali ambaye alitaka bw Kaparo kutumia uwezo wake na kuchukulia hatua za kisheria wahusika.

Rama alidai kuwa ukabila unaoendelezwa na baadhi ya viongozi wa kaunti hiyo ndio unachangia katika migororo ya chuo kikuu cha Eldoret.

Hata hivyo, Chemno alipinga madai hayo huku akitaka diwani Chomba na wenzake kuheshimu utendakazi wa afisi ya gavana.

“Sisi kama kaunti hatuandami wachuuzi kwa misingi ya kikabila kile tunataka ni kuona kuwa kuna mpangilio miongoni mwa wafanyibiashara wote hatuwezi tukaruhusu wachuuzi kufunga biashara ya watu wengine kwani watu hawa wote ni watu wetu na hatubagui watu hawa kwa misngi ya kikabila,” alisema Chemno.

Chemno aliongeza kuwa utawala wa kaunti hiyo unaendelea na mipango ya kukagua wachuuzi ili kubaini wachuuzi halali kabla ya kuondoa wachuuzi bandia katika mji huo.

Alisema kuna baadhi ya wahalifu ambao wamejificha katika wachuuzi kwa lengo la kutumia uchuuzi kuendeleza uhalifu mjini Eldoret.