Ukaguzi wa kwanza umeonyesha kuwa meli aya MV AMIN Darya iliyozamishwa baharini mwaka jana haikuwa na dawa za kulevya.
Haya ni kwa mujibu wa mkuu wa polisi wa kituo cha Kilindini, Simon Simotwa alipokuwa akitoa ushahidi wake siku ya Alhamisi kwenye kesi ya ulanguzi wa dawa za kulevya inayomkabili mwanaharakati wa kisiasa Mombasa, Maouri Abdalla Bwanamaka na wengine 12 akiwemo raia tisa wa Pakstan.
Simotwa aliiambia mahakama kuwa yeye pamoja na wenzake waliikagua meli hiyo kwa mara ya kwanza iliposhikwa baharini na hawakuona dawa za kulevya
Aidha, Simotwa aliiambia mahakama kuwa wahudumu wa meli hiyo walishirikiana nao katika kukagua meli hiyo bila usumbufu wowote.
Mwaka jana, Athuman Degereko Alfan, ambaye ni afisa wa wanamaji aliiambia mahakama kuwa aligundua meli MV Amin Darya imebeba dawa hizo baada ya kufanyiwa uchunguzi bandarini kinyume na alivyoambiwa kuwa imebeba simiti pekee.
Naye Kipkorir Keteri alitofautiana na tarehe iliyoandikwa kwenye nakala ya mashtaka, na kusema kuwa meli hiyo ilifika bandarini Mombasa Julai 3, 2014, wala si Julai 2, 2014.
Kufikia sasa mashahidi 11 wametoa ushahidi wao kwenye kesi hiyo.
Kesi hiyo inawakabili raia tisa wa kigeni kutoka Pakistan na India, na watatu kutoka Kenya ambapo wanadaiwa kunaswa na dawa za kulevya bandarini Mombasa zenye thamani ya shilingi bilioni 1.3.
Itakumbukwa meli hiyo ilizamishwa baharini na serikali mwezi Agosti 29, 2014 baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa agizo la kuchomwa kwa meli hiyo.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Januari 20,2016.