Share news tips with us here at Hivisasa

Meneja wa kampuni ya ulinzi ya kibinafsi ya Guard Force Group ameachiliwa kwa dhamana ya nusu milioni kwa tuhuma za mauwaji.

Akitoa uamuzi huo siku ya Jumatano, hakimu Julius Nang’ea alisema kuwa hakuna sababu zozote mwafaka zilizotolewa na afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma ya kutaka mshukiwa huyo kutoaachiliwa kwa dhamana, na kuongeza kuwa katiba inaruhusu mshukiwa yoyote kupewa dhamana.

Aidha, aliongeza kuwa maafisa wa polisi wamekamilisha uchunguzi wao dhidi ya kesi hiyo, hivyo basi ni vigumu kwa mshukiwa huyo kutatiza uchunguzi wowote.

Jumatano wiki iliyopita, afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa kupitia afisa wake Erick Masila waliitaka mahakama kutomuachilia Joyce Otigo kwa dhamana kwa kile alichodai kuwa atatatiza uchunguzi na kutishia mashahidi wa kesi hiyo.

Mahakama hiyo iliambiwa kuwa kati ya Oktoba 20,2015 na 26, 2015 Debra Joyce Otigo anadaiwa kushirikiana na wahalifu wengine ambao hawakuwa mahakamani kumvamia Polycarp Okum katika eneo la beach Road lililoko Kisauni wakiwa na lengo la kutekeleza mauaji hayo.

Otigo alikanusha madai hayo mbele ya hakimu Julius Nang’ea Jumatano juma lililopita.

Kesi yake itasikizwa tena Desemba 15, 2015.