Share news tips with us here at Hivisasa

Usalama mkubwa uliimarishwa katika eneo la Engashura haswa Heshima, wakati wa mazishi ya mwanabiashara mmoja wa Nakuru aliyeuawa siku chache baada ya kutekwa nyara akiwa na mwenzake.

Wawili hao Joseph Chege maarufu kama Jose na mwenzake Simon Wachira maarufu kama Shem walipatikana katika kijiji cha Gakoe, Githunguri, kaunti ya Kiambu baada ya kutekwa nyara mwezi jana, huku miili yao ikionekana kuteswa pakubwa kabla ya kuuawa.

Jose alizikwa Jumanne katika hafla iliyokuwa na ulinzi mkali, kwani polisi walihofia kwamba huenda vurumai zingezuka kwenye mazishi hayo, ikizingatiwa kulikuwa na maandamano baada ya miili ya wawili hao kupatikana.

Kulikuwa na magari manne ya polisi wa AP na GSU katika barabara kuu ya Nakuru-Subukia.

Pia usalama huo uliimarishwa kufuatia ripoti kwamba polisi wanachunguza madai ya marehemu wawili hao kuwa wafuasi wa kundi haramu la Mungiki, haswa baada ya gari lao kupatikana na silaha kulingana na polisi.

Gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua alikuwa katika mazishi hayo, ambapo alisema kwamba usalama utaimarishwa katika kaunti na kushirikiana na familia kuhakikisha waliotekeleza kisa hicho wametiwa mbaroni.