Mhudumu wa bodaboda katika eneo la Maili Sita, wadi ya Kiamaina, amelazwa katika hospitali ya Level Five mjini Nakuru akiwa na majeraha mabaya, baada ya kugongwa na matatu kwenye barabara kuu ya Nakuru-Subukia.
Ajali hiyo ilitokea kando ya ofisi za kaunti ndogo hiyo mwendo wa saa mbili asubuhi Jumapili.
Baada ya ajali hiyo, dereva alifanikiwa kutoroka, lakini polisi wa kambi ya AP ya Kiamaina wakafanikiwa kumtia mbaroni utingo wake.
“Dereva aligonga mtu huyu wa bodaboda alipogeuza gari ghafla kubeba abiria waliokuwa wanaenda mjini Nakuru, pasi na kuangalia kama nyuma yake kulikuwa na gari lingine. Hapo yeye na mtu wa pikipiki aliyekuwa nyuma ya gari wakagongana kwa upande. Ameumia kichwa na mikono, hata tulidhani amekufa kutokana na jinsi alimwaga damu barabarani," James Kamau alisema.