Mhudumu wa bodaboda ameaga dunia baada ya kuhusika kwenye ajali ya barabarani, katika barabara ya Nyamira-Konate.
Akithibitisha kisa hicho siku ya Jumatatu, OCPD wa Nyamira Ricoh Ngare, alisema mhudumu huyo alikutana na mauti pale ambapo gari la abiria lililokuwa likitoka mjini Kisii kuelekea Nyamira, lilipogongana ana kwa ana na pikipiki hiyo iliyokuwa ikiendeshwa kwa kasi.
"Mwendazake aliaga dunia baada ya pikipiki yake kugongana ana kwa ana na gari la abiria kwenye barabara ya Nyamira-Konate," alisema Ngare.
Ngare aidha alisema mwili wa mwendazake umepelekwa kuhifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali Kuu ya Nyamira, huku pikipiki na gari husika zikizuiliwa kwenye Kituo cha polisi cha Nyamira.
Ngare alisema kuwa maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali hiyo.