Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Ziara ya Rais Uhuru Kenyatta mjini Mombasa inazidi kuibua hisia kali kutoka kwa viongozi wa upinzani na sasa mbunge wa Gem Jakoyo Midiwo amejitokeza na kudai kuwa ziara hiyo haina uzito wowote wa kisiasa.

Midiwo amesema chama cha ODM kingali na umaarufu mkoani Pwani na kuwa Rais anafaa kushughulika na marekebisho ya sheria ya ardhi badala ya kuwafumba macho wakazi wa Pwani kwa kuwapa hati miliki.

"Sijaona lolote la mno alilofanya Rais katika ziara yake mjini Mombasa la kuwafanya wafuasi wetu kukihama ODM. Rais akirudi Nairobi atagundua kuwa Mombasa ingali ngome ya upinzani," alisema Midiwo.

Midiwo alidai kuwa ni kihoja kikubuwa kwa serikali kuwapa hati miliki wakazi wa Mombasa kwa shamba lao ambalo lilinyakuliwa huku akitaja hatua hiyo kama iliyopitwa na wakati.

Mbunge huyo aliongeza kuwa chama cha ODM kinajiandaa kufanya msururu wa mkutano wa kisiasa mkoani Pwani katika siku za hivi karibuni.

Midiwo alikuwa akizungumza siku ya Jumamosi katika hafla ya kuchangisha pesa katika shule ya upili ya Sirembe iliyoko katika eneo bunge lake.

Katika uchaguzi wa 2013 kiongozi wa Cord Raila Odinga alipata kura 639,246 (74.9%) mkoani Pwani, Rais Kenyatta 158,083 (19.3%) huku kiongozi wa chama cha Amani Musalia Mudavadi akipata kura 10,564 (1.3%).