Mkurugenzi mkuu wa elimu katika kaunti ya Mombasa Ibrahim Kike amesema kwamba mikakati maalum imeandaliwa kuhakikisha kwamba hakuna udanganyifu wa mitihani ya kitaifa ya KCPE.
Kulingana na Kike, tayari kamati maalum imebuni kuchunguza wanaoshirikiana na walimu pamoja na wazazi na wanafunzi kusambaza makaratasi ya uongo kwa wanafunzi kutiwa nguvuni na kufunguliwa mashtaka.
Akiongea afisini mwake na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Kike alisema kwamba maafisa wa usalama watatumwa katika kila shule ya msingi kaunti ya Mombasa kuchunguza iwapo shughuli hiyo ya udanganifu inafanyika na wahusika kutiwa nguvuni, huku akisisitiza kwamba mikati mwafaka imeimarishwa kuzuia kuchipuka kwa visa vya udanganyifu.
"Kama idara ya elimu mjini Mombasa na kaunti nzima kwa jumla tumejiandaa vyema pamoja na maafisa wetu na wale wa usalama kuhakikisha kwamba hakuna visa vya udanganyifu wa mitihani ya kitaifa inashuhudiwa, na iwapo watapatikana na udanganyifu watachukulia hatua kali za kisheria," alisema Kike.
Aidha, Kike alizidi kuwaonya wanafunzi wa shule za msingi wanaotarajiwa kufanya mitihani yao ya kitaifa ya KCPE kuwa makini na baadhi ya watu flani wanalenga kuangamiza ndoto zao za usoni, huku akisema kwamba wazingatie yale walioyasoma na kufanya vyema katika mitihani hiyo.
"Tunawaonya wanafunzi kuwa waangalifu na baadhi ya watu flani wanaolenga kuwahadaa wanafunzi na kuvuruga mitahini hiyo ya kitaifa na atakayejaribu kutumia udanganyifu basi atachukuliwa hatua za kisheria," aliongeza Kike.
Kauli ya mkurugenzi huyo mkuu wa elimu ilijiri baada ya kushuhudiwa visa vingi vya udanganyifu wa mitihani ya kitaifa ya KCSE ya shule za upili nchini, huku baadhi ya wanafunzi wakifikishwa mahakamani mjini Mombasa kwa kushiriki udanganyifu.