Mwakilishi wadi ya Lanet-Umoja, Samuel Mwangi Ngarama, amewasuta wanasiasa mahasimu wake kwa kueneza uvumi unaonuia kumharibia jina kabla ya uchaguzi wa 2017.
Ngarama alisema hayo Ijumaa akiongea na wanahabari mjini Nakuru, kufuatia madai kwamba shilingi milioni tano zilizotengwa kwa ajili ya kuweka taa za usalama maarufu kama ‘Mulika Mwizi’ katika wadi yake zimefujwa.
Alisema, “Pesa hizo zipo kwenye bajeti. Hata kama wananichukia kiasi gani, wanisubiri hadi 2017 ndio tumenyane kisiasa, lakini si kunichafulia jina kwamba nimefuja pesa za umma.”
Kulingana na Ngarama, mfumo wa utoaji kandarasi ya mradi wowote ule katika serikali ya kaunti, ni tofauti sana na unaotumika katika serikali ya kitaifa.
“Wananchi ndio hutoa mapendekezo ya miradi wanayotaka ipewe kipau mbele, kisha wahandisi wa kaunti wanakagua kiasi cha pesa zitakazotengewa miradi hiyo, na hatimaye zinatangazwa kwa umma,” alisema Ngarama.
Aliongeza kuwa ‘CDF huwa hawana mpangilio kama huo wa kaunti na ndio maana miradi yao inaweza kuharakishwa’.
Hata hivyo alisema taa hizo zitakuwa tayari kabla ya mwaka huu kutamatika.