Mitaa kadhaa katika Kaunti ya Nairobi itakumbwa na uhaba wa maji kuanzia siku ya Jumatatu hadi Jumamosi kwa minajili ya kutoa nafasi kwa ukarabati wa bomba linalosafirisha maji kutoka bwawa la Sasumua hadi hifadhi ya maji iliyoko eneo la Kabete.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumamosi, kampuni ya Maji ya Nairobi imesema ukarabati huo unaoendeshwa katika msitu wa Aberdares unalenga kuimarisha usambazaji wa maji jijini Nairobi na viunga vyake.
Maeneo yatakayoathirika ni mitaa ya Kangemi, Westlands, Parklands, Hospitali ya MP Shah, Aga Khan na eneo la Community.
Vile vile, mabweni ya bewa kuu la Chuo Kikuu cha Nairobi na mabewa ya Upper Kabete, Lower Kabete na Parklands yatakosa maji kwa saa kadhaa katika kipindi hicho.
Mitaa mingine itakayoathirika ni mtaa wa Kibera, Jamhuri, Riruta Satelite, Dagoreti Corner, Kawangware, Langata na Karen.