Mizoga ya mbuzi saba waliopotea katika eneo la Mwisyani, Kaunti ndogo ya Matungulu, imepatikana nje ya pango moja katika eneo hilo.
Mbuzi hao waliopotea usiku wa kuamkia siku ya Jumatatu wanashukiwa kuliwa na fisi baada ya nyayo za fisi kupatikana katika eneo hilo.
Akidhibitisha kisa hicho, naibu wa chifu wa Nguluni Virginia Mweu alisema kuwa habari zilizofika ofisini mwake ni kuwa mbuzi wasaba walikuwa wamepotea, lakini baada ya uchunguzi kuanzishwa, mizoga ya mbuzi hao ilipatikana nje ya pango moja.
"Siku mbili zilizopita, mbuzi wasaba waliripotiwa kupotea ambapo kila mtu alidhani walikuwa wameibiwa kabla ya mizoga hiyo kupatikana. Mizigo hiyo imetapakaa nje ya pango moja anbalo lilikuwa makao ya fisi miaka ya themanini,” alisema Mweu.
Vilevile, chifu huyo aliwaomba wakazi wanaohofia maisha yao kuwa watulivu kwa kuwa maafisa wa wanyamapori wametia mitego nje ya pango hilo ili kuwakamata fisi hao.
"Askari wa wanyamapori waliarifiwa kuhusu kisa hicho na walifika hapo na kutia mitego ya kuwakamata fisi hao. Kwa hivyo ningewaomba watu wasiwe na hofu kwani shida hiyo itatatuliwa,” alisema Mweu.