Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, amegadhabishwa na mwamko mpya wa upishi na uuzaji wa pombe haramu eneo hilo.
Kimani amesema polisi wanazembea katika kuhakikisha pombe hizo zimemalizwa, huku madai yakitolewa kwamba wakuu wa nyumba kumi wanaojaribu kupigana nayo wanahangaishwa na polisi hao.
“Niliongoza kumwaga chang’aa wakati wa oparesheni iliyoanzishwa na rais, nikasema afadhali nipoteze kura lakini watoto wetu wapate nafuu. Sitachelewa kuanzisha oparesheni maliza chang’aa awamu ya pili,” akasema Kimani.
Wakati uo huo Kimani ametahadharisha wakaazi wa eneo hilo dhidi ya kulaghaiwa na madalali wa stima kupitia mradi wa ‘Angusha Stima’.
Angusha stima ni mradi ambao uliwapa wakaazi hao fursa ya kupata umeme nyumbani mwao kwa bei isiyozidi Sh1,060.
Walionufaika na mradi huo ni wale ambao walikuwa umbali usiozidi mita mia sita kutoka kwa laini ya umeme, mpango uliofanikishwa kwa ushirikiano wa serikali kuu, shirika la kusambaza umeme nchini KP, ofisi yake, na wafadhili wengine.
Lakini kulingana na mbunge huyo, watu Fulani walikuwa wakiwalaghai wananchi kwa kuwaitisha kati ya Sh5,000 na Sh8,000 ili kuunganishwa na stima. Wanaitishwa hadi shilingi elfu 15.
“Hakuna kitu unafaa kulipa kuwekewa umeme kupitia Angusha Stima, mradi tu nyumba yako umeweka nyaya za stima. Hizo shilingi elfu moja na stini, unatakiwa kulipa kupitia bili yako ya stima kila mwezi shilingi 99 pekee,” akasisitiza mtunga sheria huyo.