Mke wa gavana wa kaunti wa Nyamira Naomi Nyagarama amewaomba wahisani kusaidia watu zaidi ya elfu thelathini katika eneo hilo wanaoathirika na funza kama njia mojawapo ya kuwasaidia kuimarisha maisha yao.
Nyagarama ameongeza kwa kusema kuna haja ya wahisani kujitokeza na kuwasaidia maskini kwenye jamii ili kuwawezesha kujikimu kimaisha kwa kuwa wengi wa wanaoathirika na funza pia wanakosa nguo, blanketi na chakula kwa sababu ya umaskini unaowakumba.
"Funza zimewaathiri watu wetu walio na umaskini, na wakati umefika sisi sote kupambana na shida ambayo imekuwa janga kuu," alisema.
Nyagarama, ambaye aliandama na mwakilishi wa wadi ya Mekenene Alfayo Ngeresa alikuwa akizungumza katika shamba la majani chai ya Kipkebe na Keritor kwenye kaunti ndogo ya Borabu siku ya Jumatatu, ambako alitoa viatu kwa wafanyakazi na watoto wao.
Alisema viatu hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni mbili vilitolewa na shirika lisilo la kiserikali la Ahadi Kenya Limited, akiongeza kuwa vilivyobaki vitapewa wakazi wa kaunti hiyo maskini walio na umri wa zaidi ya miaka 70.
"Viatu ambavyo tumevipeana hii leo ni vya thamani ya shillingi millioni mbili, na ni kupitia ufadhili wa shirika la Ahadi Kenya," alisema Nyagarama.