Mkurugenzi mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la HAKI Afrika Hussein Khalid amepongeza uamuzi uliofanywa na mahakama kuu ya Mombasa ya kuagiza kufunguliwa kwa akunti za benki za shirika hilo na lile la MUHURI.
Kwenye taarifa yake aliyoituma katika vyumba vya habari siku ya Alhamisi, Khallid alisema hatimaye haki imepatikana kwa mashirika hayo.
Khalid alisema wanafurahia uamuzi huo ambao amesema umetia kikomo changamoto nyingi ambazo wamekuwa wakipitia kama shirika kwa kipindi cha muda wa miezi minane.
Aidha, aliongeza kuwa kufikia sasa, idara ya mahakama imeonyesha mfano mzuri kwa jamii kwa uamuzi huo.
Zaidi alisema kuondolewa kwa mashtaka hayo kumewapa motisha na nguvu za kuendelea na kazi yao ya kutetea haki za binadamu katika taifa hili la Kenya.
Siku ya Alhamisi, jaji Anyara Emukhule wa mahakama kuu ya Mombasa ilitoa agizo la kufunguliwa kwa akaunti za benki za mashirika mawili ya kutetea haki za kibinadamu mjini Mombasa kwa kusema kuwa kufungwa kwa akaunti hizo ni kinyume cha katiba.
Mashirika hayo mawili yalifungiwa akaunti zao kwa madai ya kuhusishwa kufadhili makundi ya Kigaidi.
Mashirika hayo ni miongoni mwa mashirika na akaunti za watu 85 zilizofungwa na serikali kwa tuhumza za kufadhili makundi ya kigaidi nchini siku chache tu baada ya tukio la kigaidi la chuo cha Garisa lililopelekea watu 148 kuaga dunia na wengine 79 kupata majeraha.