Afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma imetaka kulipwa fidia kwa familia ya mtoto wa miaka 14 mwendazake Kwekwe Mwandaza aliyepigwa risasi mwaka 2014.
Kupitia naibu wake tawi la Mombasa Alexedra Muteti, aliambia mahakama kuu ya Mombasa siku ya Ijumaa, kuwa familia hiyo inafaa kulipwa fidia ikizingatiwa ilipoteza mpendwa kutokana na kupigwa risasi kiholela na maafisa wa polisi.
Kauli yake iliungwa mkono na wakili wa familia hiyo Haron Ndubi kwa kusema kuwa fidia hiyo itagharamia ada ya mazishi na ada ya kesi hiyo.
Naye wakili wa washtakiwa Gerad Magolo ameitaka mahakama kuwapa kifungo cha nje wateja wake ili waweze kulipa fidia hiyo.
Aidha, ameiambia mahakama kuwa wateja wake wako na familia changa na iwapo watafungwa basi familia zao zitapata shida za kiamaisha.
Itakumbukwa siku ya Jumatano jaji Martin Muya aliwapata na kosa la mauwaji ya Kwekwe bila kukusudia maafisa Veronica Gitahi na Issa Mzee mnamo Agosti 22 mwaka 2014 katika kijiji cha Maweu huko Kinango kaunti ya Kwale.
Mahakama kuu itatoa hukumu ya kifungo na kiwango cha fidia siku ya Jumatatu wiki ijayo.