Mkurugenzi wa huduma za Feri ya Likoni Musa Hassan Musa ameachishwa kazi kutokana na kile kinaaminika kuwa shinikizo kutoka kwa wadau.
Musa alifutwa kazi siku ya Jumatano, siku mbili tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuzuru kivuko cha feri na kuonyesha kutoridhishwa kwake na huduma zinazotolewa na usimamizi japo hakuamuru yeyote kuachishwa kazi.
Mkurugenzi huyo amekuwa chini ya shinikizo kwa muda sasa huku viongozi mbali mbali akiwemo kiongozi wa vuguvugu la 'Pwani ni Kenya' Alex Kasuku na hata kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa wakitaka aachishwe kazi huku wakidai kuwa ameshindwa kuwajibika ipasavyo.
Huduma mbovu pamoja na misongamano ya mara kwa mara inayoshuhudiwa katika kivuko hicho ni miongoni mwa mambo yanayoaminika kuchangia mkurugenzi huyo kufutwa kazi.
Hata hivyo, kulingana na stesheni moja ya humu nchini inayodai kuzungumza naye baada ya taarifa hizo kuchipuka, Musa amekana kufutwa kazi huku akisema alijiondoa kufuatia muda wake wa kuhudumu katika shirika hilo kutamatika.
Hadi wakati wa kuandika taarifa hii, usimamizi wa huduma za feri ya Likoni haukuwa umetoa taarifa rasmi kuthibitisha kuwa mkurugenzi wake amefutwa kazi.