Mkurugenzi mkuu wa Halmashauri ya Bandari ya Mombasa, Gichiri Ndua, ameachishwa kazi na serikali kwa kile kimetajwa kama hatua inayolenga kuvikabili visa vya ufisadi katika bandari hiyo.
Kwenye kikao na wanahabari katika Jumba la Harambee mjini Nairobi siku ya Jumanne, waziri wa uchukuzi, James Macharia, akiandamana na waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery, alithibitisha kufutwa kazi kwa Gichiri siku moja tu baada ya bodi ya KPA kusitisha kandarasi yake iliyotarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka huu.
Kando na Gichiri, wengine walioachishwa kazi ni pamoja na meneja mkuu wa Bandari Twalib Khamisi, mshauri wa masuala ya kisheria Muthoni Gatere, mkuu wa kitengo cha ushirika Justsus Nyarandi pamoja na mkuu wa usalama Mohamed Morowa.
Kamishna mkuu wa Halmashauri ya ukusanyaji ushuru nchini KRA, John Njiraini, ambaye pia alikuwa katika kikao hicho alisema kuwa maafisa wengine waliokua wakihudumu bandarini humo pia wamepewa uhamisho.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya kamati iliyotikwa jukumu na Rais Uhuru Kenyatta kutathmini utendakazi wa viongozi wa bandari hiyo kukamilisha uchunguzi wake na kutoa pendekezo.
Kwa muda sasa, usimamiza wa Bandari ya Mombasa umelaumiwa kwa visa vya ufisadi ambavyo vimechangia uingizaji wa bidhaa ghushi nchini kupitia Bandari hiyo.