Share news tips with us here at Hivisasa

Mkuu wa polisi wilayani Kenyenya, eneo bunge la Bomachoge Borabu Leonard Baini amekosolewa vikali kwa kutotoa huduma kwa wakazi wa wilaya hiyo jinsi inavyostahili.

Hii ni baada ya mkuu huyo wa polisi kutumia ofisi iliyoko katika mji wa Ogembo, na kuiacha ile iliyoko wilayani Kenyenya ambayo ndio iko karibu na wananchi wengi.

Akizungumza siku ya Jumatano katika wadi ya Bokimonge, Mwakilishi wa wadi hiyo George Bibao alimkosoa mkuu huyo wa polisi huku akisema kama hayuko tayari kurudi katika ofisi yake iliyoko wilayani Kenyenya basi yuko na fursa ya kupewa uhamisho hadi wilaya tofauti kwani hayuko tayari kufanya kazi kwa wakazi wa Kenyenya.

“Tulipigania mji wa Kenyenya hadi ukainuka na kukabidhiwa wilaya na mkuu wa polisi akatumwa hapa ili kuwahudumia wakazi kwa masuala ya usalama, lakini mkuu huyo wa polisi hutumia ofisi iliyoko mjini Ogembo na hapo ni mbali na katika eneo tofauti,” alisema Bibao.

“Wakazi hawawezi kutembea hadi Ogembo kutafuta huduma, hiyo huwa vigumu sana. Mambo ya usalama ni jambo la muhimu kwa wakazi, tunastahili kuwa na mkuu wa polisi hapa Kenyenya kwani ofisi yake iko tayari hapa,” aliongeza Bibao.

Sasa mwakilishi wadi huyo amemtaka mkuu huyo wa polisi kurudi katika wilaya ya Kenyenya na kutumia ofisi iliyoko mjini humo.

Mkuu huyo wa polisi alienda kuitumia ofisi iliyoko mjini Ogembo kwa kuwa wakati huo hakukua na ofisi wilayani Kenyenya, lakini baadaye ofisi hiyo ilijengwa na kukamilika huku akihitajika kurudi na kuanza kuitumia.