Mlinzi mmoja wa kivuko cha feri amejipata pabaya baada ya kushambuliwa kwa ngumi na mateke alipokuwa akijaribu kuzuia abiria waliokuwa na ghadabu baada ya feri ya MV Harambee kukwama.
Jambo liliwalazimu walinzi wenzake kuingilia kati na kumwokoa kutoka kwa kichapo hicho, na kwa bahati njema, hakupata majeraha yoyote kutokana na kipigo hicho.
Mlinzi huyo alipatana na masahibu hayo alipokuwa akijaribu kuzuia msongamano wa abiria waliokuwa wakiingia ndani ya feri kutoka sehemu mbali mbali siku ya Jumanne asbuhi.
Hii ni baada ya msongamano mkubwa wa watu kushuhudiwa kwa mara nyingine tena katika kivukio cha Likoni, ukiwa umesababishwa na kukwama kwa Feri ya MV Harambee.
Kutokana na walioshudia kisa hicho, wakiongozwa na Martin Kimani, usimamizi wa shirika la feri linajikokota kutatua tatizo hilo la kila mara.
Aidha, ameongeza kuwa walinzi wa kivuko hicho wanafaa kufunzwa jinsi ya kushughulikia abiria, wala si kuwa na kiburi kama walivyo.