Kijana mmoja alifariki na mwingine kujeruhiwa kupitia ajali ya barabarani siku ya Jumanne baada ya gari aina ya probox kupoteza mwelekeo katika eneo la Nyatieko katika barabara kuu ya Kisii-Kegogi na kugonga kijana huyo wa umri wa miaka 16 kando mwa barabarana kufariki papo hapo.
Inasemekana kuwa kijana huyo alikwa katika shughuli zake za kusomba kokoto katika eneo la Nyatieko,kabla ya gari hilo kupoteza mwelekeo na kumgonga na kufariki papo hapo, na kisha kumjeruhi mwanamke ambaye alikuwa karibu na kisa hicho.
Kulingana na walioshuhudia ajali hiyo, dereva wa gari hilo aina ya probox alitoroka baada ya kisa hicho kutokea na hadi sasa hajapatikana aliko
Pia wasafiri waliokuwa kwa gari hilo walinusurika kifo na majeraha madogo madogo, huku wengine wakitafuta njia mbadala na kuendelea na safari yao.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne baada ya ajali hiyo walioshuhudi ajali hiyo walisema gari hilo aina ya probox lilikuwa likiendeshwa kwa kasi, ndiposa likapoteza mwelekeo kabla ya kusababisha ajali hiyo.
“Gari hili lilikuwa na abiria ndani ingawa lilikuwa linaendeshwa kwa kasi na kupoteza mwelekeo na kugonga kijana mmoja na mwanamke mmoja hapa kando kando mwa barabara,” alisema Charles Mokua .
Mwanamke aliyejeruhiwa alipelekwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii kwa matibabu, huku marehemu akipelekwa katika chumba cha kuifadhi maiti cha Kisii .
Wakazi hao wamewataka madereva kuwa waangalifu kila mara wanapokuwa barabarani kwa shughuli za uchukuzi
Maafisa wa polisi wa kituo cha Marani na wale wa Nyatieko walichukua gari hilo hadi kituo cha polisi cha Kisii huku uchunguzi ukiendelea.